
858
MKMkoa wa Songwe unaendelea kuvutia wawekezaji katika sekta ya kilimo baada ya kupokea ugeni wa wawekezaji wa zao la soya kutoka kampuni ya Mount Meru wakiongozana na Mkurugenzi Mkuu wa taasisi ya COPRA, Bi. Irene Mlola pamoja na Mkurugenzi wa Mazao kutoka Wizara ya Kilimo.
Ziara hiyo iliongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mheshimiwa Jabiri Omari Makame tarehe 20 Aprili 2026, ikiwa na lengo la kutembelea maeneo yaliyotengwa kwa uwekezaji wa zao la soya katika Wilaya za Momba na Mbozi.
Katika ziara hiyo, wawekezaji walioneshwa eneo la hekari 118 katika Kata ya Myunga, Wilaya ya Momba pamoja na hekari 561 katika Wilaya ya Mbozi kwa ajili ya uwekezaji wa zao hilo.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Songwe Mheshimiwa Jabiri Omari Makame aliahidi ushirikiano wa kutosha kwa wawekezaji ili kuhakikisha uwekezaji huo unatekelezwa kwa mafanikio na kuchochea ajira pamoja na ukuaji wa uchumi wa wananchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa COPRA, Bi. Irene Mlola alisema taasisi hiyo ipo tayari kuwekeza katika mnyororo wa thamani wa zao la soya kwa kuongeza uzalishaji, usindikaji na masoko jambo litakalowanufaisha wakulima wa Mkoa wa Songwe.
Aidha, Wizara ya Kilimo imeeleza mkakati wake wa kuanza na soko kwanza ili kuongeza tija kwa wakulima na kuhakikisha uzalishaji unaendana na mahitaji halisi ya soko.
Hatua hii inatarajiwa kufungua fursa mpya za ajira na kuongeza kipato kwa wakulima wa zao la soya mkoani Songwe.
#Songwe #KilimoBiashara #Uwekezaji #Soya #Ajira MaendeleoYaWananchi
@mkoa_wa_songwe










